Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Tukio la Ghadir Khum linaendelea kukumbukwa na mamilioni ya Waislamu duniani kama moja ya matukio makubwa katika historia ya Uislamu, ambapo Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alimshika mkono
Imam Ali ibn Abi Talib (a.s) na kuuinua mbele ya umati mkubwa wa mahujaji waliokuwa wakirejea kutoka Hijjatul-Widaa.
Katika tukio hilo maarufu, Mtume (s.a.w.w.) alinukuliwa akisema: "Yeyote ambaye mimi ni Mola wake, basi Ali ni Mola wake." Tamko hilo lilitolewa katika eneo la Ghadir Khum mbele ya maelfu ya Waislamu, likisisitiza nafasi maalumu ya Imam Ali (a.s) katika kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya Mtume.
Kwa mujibu wa mapokezi mengi ya Kiislamu, baada ya tangazo hilo iliteremshwa Aya ya Qur'ani inayosema:
"Leo nimekukamilishieni dini yenu, nimewatimizieni neema Yangu, na nimeuridhia Uislamu kuwa dini yenu." (Al-Ma'idah: 3)
Wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s) wanaamini kuwa aya hii iliteremshwa kuashiria ukamilifu wa dini kupitia kutangazwa kwa uongozi wa Imam Ali (a.s), huku tukio la Ghadir likichukuliwa kuwa msingi wa uendelezaji wa ujumbe wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) baada ya kufariki kwake.
Kila mwaka, waumini katika maeneo mbalimbali duniani huadhimisha Sikukuu ya Ghadir kwa kufanya mikusanyiko ya kidini, mihadhara na shughuli za kijamii zinazolenga kuhuisha mafundisho ya uongozi, uadilifu na mshikamano yaliyoasisiwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt wake watoharifu.
Your Comment